MSIBA BULYANHULU

Waliofukiwa Bulyanhulu waopolewa wamekufa
na Stella Ibengwe, Shinyanga


JUHUDI za kuwaokoa wafanyakazi watatu wa mgodi wa Bulyanhulu katika Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, walioangukiwa na kifusi wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji hazikuzaa matunda jana, baada ya kuwakuta wote wakiwa wamefariki dunia.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kahama, Meja mstaafu Bahati Matala, ambaye alikuwa mmoja wa viongozi waliokesha katika zoezi hilo, alisema zoezi hilo lilifanyika katika hali ya uangalifu mkubwa, ingawa wafanyakazi wote walikutwa wamefariki dunia baada ya kukosa hewa.
Meja Matala aliwataja waliofariki dunia kuwa ni pamoja na Dickson Kaderema, ambaye alikuwa akiendesha mashine aina ya Jumbo.
Alisema wakati zoezi la uokoaji lilipokuwa likiendelea sauti zao zilikuwa zikisikika, lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda zilipotea ghafla.
Aliwataja wafanyakazi wengine waliofariki dunia kuwa ni Martin Joel na Vedastus Tanbise.
Awali taarifa zilizopatikana zilisema kulikuwa na wafanyakazi 30 ndani ya mgodi, ambao waliweza kunusurika katika tukio la kufukiwa na kifusi.
Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Kakola, Bugarama na Ilogi, waliliambia gazeti hili kuwa waliingiwa simanzi ghafla baada ya kupata taarifa za tukio hilo, ingawa hawakuruhusiwa na mamlaka husika kwenda kusaidia kazi ya uokoaji.
Inasadikiwa baada ya mwamba kuporomoka uliangukia mashine aina ya Jumbo, hivyo kuwabana wafanyakazi hao, hali iliyosababisha kushindwa kujiokoa.
DC huyo alisema shughuli za uchimbaji hadi jana zilikuwa bado zimesimamishwa hadi taarifa ya uongozi wa mgodi itakapotolewa.

No comments: