UBABE WA DOLA ARUSHA


10 wauwawa kwenye ghasia mjini Arusha
.....Dr Wilbroad Slaa naye pia amekamatwa

Watu wasiopungua kumi wameripotiwa kuuwawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mji wa Arusha Tanzania, kwenye makabiliano baina ya Polisi na wafuasi wa chama cha upinzani cha CHADEMA.

Ghasia zilianza baada ya Polisi kumkamata mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Freeman Mbowe na mbunge wa Arusha mjini Godbless Jonathan Lema, wakiwa wanaelekea kuhutubia mkutano wa kisiasa.

Baadaye polisi pia walimkamata aliyekuwa mgombea wa chama hicho cha CHADEMA kwenye uchaguzi wa Urais uliofanyika mwezi Oktoba Dr Wilbroad Slaa.

Taarifa zinasema biashara kadhaa zilichomwa moto kwenye vurugu hizo.
Kwa mujibu wa waandishi wa habari mjini Arusha, Polisi walikuwa wamewakataza viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao kufanya maandamanao kabla ya mkutano wa kisiasa wa Jumatano, lakini mamia ya wafuasi wa chama hicho wakawafuata viongozi hao walipokuwa wanaelekea eneo la mkutano.

Bwana Slaa amenukuliwa akisema maandamano hayo yalikuwa ya kupinga ufisadi katika serikali mpya ya Rais Jakaya Kikwete.

Polisi walifyatua risasi hewani mara kadhaa kutoa tahadhari kwa maelfu ya wafuasi waliokwenda kutaka viongozi wao waachiwe huru, na baadaye wakafyatua gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya.

Walioshuhudia wanasema Polisi waliendelea kufyatua risasi mchana kutwa, huku wafuasi wa CHADEMA wakiendelea kukabiliana na askari Polisi katika maeneo mbali mbali ya mji wa Arusha.

Kwenye mkutano huo wa kisiasa, Dr Slaa aliwataka Polisi kumwachilia huru Bwana Mbowe na wengine, na pia akamtaka Rais Kikwete kujiuzulu.

Hadi kufikia Jumatano jioni hakuna taarifa iliyokuwa imetolewa na serikali kuhusu mzozo huo.
Kumekuwa na mvutano wa kisiasa nchini Tanzania tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Urais ambao vyama vya upinzani vinadai ulikuwa na udanganyifu.

Kufuatia uchaguzi huo shinikizo zinaendelea za kutaka Tanzania iwe na katiba mpya tofauti na iliyopo sasa, ambayo hairuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais kupingwa mahakamani yanapotangazwa na tume ya uchaguzi.

No comments: